Jumapili , 28th Jul , 2024

Wanamichezo watatu wa Tanzania walioko Paris kwenye michezo ya 33 ya Olimpiki ya majira ya joto ya Paris 2024 wameendelea na mazoezi makali chini ya makocha wao, wakijiandaa kwa michuano yao inayoanza rasmi kesho Jumatatu Julai 29, 2028.

Tanzania itatupa karata yake ya kwanza kwenye michuano hii ya 33 ya Olimpiki ya Majira ya joto kesho Jumatatu Julai 29, 2024 wakati mchezaji wake wa Judo, Andrew Thomas Mlugu,  atakapopanda ulingoni kupambana na William Tai Tin, judoka wa kutoka nchi ya Samoa. Mpambano wao utakuwa saa 5 asubuhi kwa saa za Tanzania.
 
Tai Tin anatoka Siumu na Kisiwa cha Manono lakini anaishi Melbourne, Australia, na alikuwa sehemu ya timu ya Samoa katika  Michezo ya Jumuiya ya Madola ya 2022 huko Birmingham. Ana umri miaka 39.
 
Siku ya pili, yaani  Jumanne Julai 30, 2024 Tanzania itatupa karata yake ya pili wakati muogeleaji Collins Phillip Saliboko, atakapoingia bwawani kushindana katika mita 100 (Freestyle) kwa wanaume mnamo saa 6:15 mchana kwa saa za Tanzania.
 
Karata ya tatu ya Tanzania itatupwa Jumamosi Agosti 3, 2024 na mwogeleaji Sophia Anisa Latiff ambaye atashindana katika mita 50 (Freestyle) kwa wanawake mnamo  saa 6:00 mchana kwa saa za Tanzania.