Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam,Mkurugenzi wa Sheria wa Yanga SC Simon Patrick amesema wameiomba Mahakama kuwaongezea muda kuhusu shauri hilo huku akiwaondoa wasiwasi kuhusu uhalali wa uwepo wa Rais wa Yanga Injinia Hersi na kamati ya Utendaji ndani ya Yanga SC
"Mnamo tarehe 6/11/2022 watu wawili waliojiita Wanachama wa Young Africans SC walifungua kesi Mahakama ya Kisutu, Bwana. Juma Ally pamoja na Geofrey Mwipopo. Walifungua kesi dhidi ya Wajumbe wa Baraza la Wadhamini ambao ni Mama yetu Fatma Karume, Abeid Mohamed Abeid na Mzee Jabir Katundu kwa madai ya kuwa hawalitambui baraza la wadhamini la Klabu ya Young Africans SC, wakidai liliingia kwa mujibu wa Katiba ya 2010(ambayo wanadai haijasajiliwa)" Simon Patrick - Mkurugenzi wa Sheria wa Young Africans
Kwa upande mwingine,Patrick Simon amesema klabu ya Yanga SC haitosita kuwachukulia hatua ya kinidhammu kwa Wanachama wote wanaotaka kuivuraga Yanga huku tayari wamepanga kufungua kesi ya jinai kwa Abeid Mohamed Abeid kwa kosa la kugushi saini za klabu pamoja na saini za baraza la wadhamini wa klabu ya Mama Fatma Karume na Mzee Jabir Katundu
"Klabu tumegundua kuwa, Abedi Mohamed Abedi aligushi sahihi za Mama Fatma Karume, alighushi sahihi Jabir Katundu ambaye alilazimishwa na sahihi ya Mzee Mkuchika. Mzee Jabir Katundu alituma barua yake Kisutu akieleza kuwa hakuwahi kusaini chochote kinachohusiana na kesi hiyo.
Klabu imeomba Mahakama iongeze muda wa Klabu kufanya mapitio ya kesi kwani Klabu haikuwahi kushiriki kwenye kesi hiyo. Klabu vile vile itaomba mahakama ifuatilie jinai ambazo zimeonekana kwenye kesi hiyo ikiwemo kughushi sahihi za baadhi ya Viongozi waandamizi wa Young Africans SC" Simon Patrick - Mkurugenzi wa Sheria
Sakata hili la Yanga SC linakuja baada ya Wanachama wawili wa Yanga SC Juma Ally Magoma na Geofrey Mwaipopo kufungua kesi kwenye Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu mnamo Agosti 4-2022 dhidi ya Baraza la Wadhamini wa Yanga SC kuhusiana na matumizi ya katiba ndani ya klabu hiyo.