Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga (kulia) akipokea nyaraka mbalimbali kuhusu mkakati wa kampuni ya Taifa Gas katika kufanikisha suala zima la upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ya gesi kutoka kwa Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Devis Deogratius wakati maofisa wa kampuni hiyo walipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana.
Mitungi hiyo iliyopokelewa hivi karibuni na Makamu wa Rais Dk. Phillip Mpango, ilitolewa na kampuni ya Taifa Gas ikilenga kuunga mkono kampeni ya kumtua mama kuni kichwani inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Kampeni hiyo inalenga kuwasaidia na kuwawezesha wananchi kuifikia nishati hiyo kwa urahisi.
Kapinga alitoa ahadi hiyo katika kikao chake na maofisa waandamizi wa kampuni ya Taifa Gas wakiongozwa na Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Devis Deogratius walipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana.
Pamoja na kuipongeza kampuni hiyo kwa juhudi zake za kuunga mkono kampeni ya kumtua mama kuni kichwani Kapinga alisema ufanisi wa kampeni hiyo unategemea zaidi ushiriki wa wadau wengi zaidi kwa kuzingatia ukweli kwamba kampeni hiyo inalenga kuwafikia walengwa kote nchini.
“Kama wizara, tumedhamiria kuhakikisha kwamba tunawafikia walengwa wote wanaostahili kufikiwa na kampeni hii kama ambavyo Rais Samia alivyokusudia. Kwetu imekuwa faraja kubwa kuona wadau kama Taifa Gas wapo nasi bega kwa bega kuhakikisha hilo linafanikiwa. Pamoja na kusambaza mitungi hii ya gesi pia tutahakikisha elimu kuhusu nishati safi ya kupikia inawafikia walengwa kila wilaya na kila kata,’’ alisema Kapinga.
Aidha, Kapinga alitoa wito kwa kampuni ya Taifa Gas kuhakikisha kuwa inaongeza zaidi vituo vya kujazia gesi katika maeneo mbali mbali nchini, ili wananchi wengi zaidi waweze kufikiwa na huduma ya nishati hiyo kwa urahisi.
Kwa upande wake Deogratius alisema kuwa Taifa gas itaendelea kushirikiana na serikali katika kuimarisha kampeni ya matumizi ya nishati safi, huku akibainisha kwamba kampuni hiyo itaendelea na mkakati wake wa kupanua zaidi uwekezaji wake kwenye maghala yake nchini, ili kuihakikishia nchi usalama na upatikanaji wa nishati hiyo.
“Tunaelewa kuwa mabadiliko kuhusu matumizi ya nishati yanaendelea kuonekana na yatakuwa taratibu. Cha msingi ni kuweka mikakati ya kuongeza idadi ya watumiaji wa nishati safi nchini kutoka asilimia nane ya sasa,” alisema Deogratius.
Miongoni mwa maeneo ambayo yamelengwa na kampeni hiyo ni maeneo ambayo yameathirika kwa kiasi kikubwa na janga la ukataji wa miti kama vile mkoa wa Iringa na maneo mengine.