Jumatatu , 5th Feb , 2024

Viongozi wa CCM Mkoa Tanga wametakiwa kukosoa pale wanapoona usimamizi wa shughuli za serikali zinasuasua kutokana na uzembe wa watendaji ambao unachangia kuchafua chama hicho na kukihatarisha kwenye chaguzi zake. 

Kauli hiyo imetolewa na viongozi wa chama cha mapinduzi kwenye maadhimisho ya sherehe ya miaka 47 tangu kuanzishwa kwa chama hicho zilizofanyika katika kata ya Mayomboni Wilaya ya Mkinga. 

Viongozi hao akiwemo mjumbe wa Kamati ya siasa ya CCM Mkoa Tanga Omary Ayoub amesema kuwa viongozi wa ccm hawatakiwi kukaa mbali na kutizama utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuwa mtendaji akifanya makosa anakichafua chama cha mapinduzi licha ya kwamba serikali imekuwa ikitoa huduma kwa wananchi wake. 

"Viongozi wa ccm kwenye kata zetu na vijiji vyetu mna haki ya kuyasemea na kukosoa yale ambayo hayafanyiki kwa usahihi na ndio maana tumepewa dhamana ya kuliongoza Taifa hili asiyetaka aache kazi,  asiyependa rangi ya kijani kwenye ofisi yake aache kazi,  wakati tunacheza ngoma kuomba kura wao walikuwa wamepumzika tunapotaka majibu kuhusu wananchi wetu wanatakiwa watoe majibu kusiwe na masimango, "alisema Ayoub. 

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya siasa Wilaya Ya Mkinga Twaha Mwakioja amewataka wananchi kuhakikisha hawakosei katika kuchagua viongozi kwani kufanya hivyo kutawakosesha haki zao za msingi. 

Naye Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa Tanga Omary Ramadhani amesisitiza viongozi wote waliopewa dhamana katika vipimdi vyote vya uchaguzi ikiwemo serikali za mitaa,  madiwani na wabunge kabla ya kufanya maamuzi ya kwenda kuchukua fomu wajitafakari na kujitathimini kwa kina wamewezaje kuwatumikia wananchi waliowapa ridhaa. 

"Wewe Mwenyekiti wa serikali ya mtaa kama ulikuwa chanzo cha migogoro katika maeneo yako,  kama diwani ulikuwa chanzo cha migogoro katika kata yako wewe Mbunge kama ulikuwa ni chanzo cha migogoro katika jimbo lako 2024 Mwenyekiti wa serikali ya mtaa usithubutu kwenda kuchukua fomu sababu jina lako halitarudi,  2025" alibainisha Ramadhani.