Jumamosi , 9th Dec , 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na serikali kuwahifadhi waathirika wa Maporomoko ya Mawe na Matope kutoka Mlima Hanang’ mkoani Manyara.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa kikao na viongozi wa Serikali, Wazee na Waathirika wa Maporomoko hayo katika Kijiji cha Gendabi Halmashauri ya wilaya ya Hanang’ Mkoani humo.

Waziri Mhagama amewakumbusha kuwa Serikali itaendelea kutoa huduma zote muhimu kwa kila aliyeathirika na maafa hayo na kipaumbele ni wale waliohifadhiwa katika Kambi za muda zilizopo na endapo kuna mazingira rafiki ya kuhifadhiwa na ndugu, jamaa na marafiki wanapaswa kufuata utaratibu zilizopo.

Aidha alishauri kuwa, Wananchi wawapokee waathirika wa Maporomoko ya Mawe katika makazi yao na hata kama nyumba itakuwa haitoshi serikali itawezesha kujenga mahema ili waweze kujitosheleza.

Alifafanua zaidi kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha vifaa vya msaada wa kibinadamu vinawafikia waathirika katika maeneo yao kwa kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu ikiwemo chakula, magodoro pamoja na mablanketi.

Kwa upande wake Nyerere Izrael Mwenyeji wa kijiji cha Gendabi ameomba serikali kutuma wataalamu kuangalia tabia za Mlima Hanang’ ili janga hilo lisije likajirudia.