Jumatano , 22nd Nov , 2023

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Anna Henga kimetoa mapendekezo yake ya jumla ili kuboresha miswada mitatu iliyowasilishwa Bungeni hivi karibuni

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Dkt. Anna Henga (Wakili) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo kwenye picha) wakati akitoa maoni ya jumla kituo hicho juu ya Miswada mitatu ya Seheria ya Uchaguzi iliyowasilishwa Bungeni hivi karibuni.

Miswada mitatu iliyowasilishwa ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Vyama vya Siasa na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Akizungumza na wanahabri Dkt. Henga amesema pamoja na uchambuzi uliofanyika, mapendekezo ya jumla ya LHRC ni pamoja na kujumuishwa haki ya wafungwa kupiga kura kwa utaratibu utakaowekwa kwa sheria kama ilivyoamuliwa na Katiba kufanyiwa marekebisho kwa kuweka mfumo wa usaili wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi.

Aidha Dkt. Henga amesmea LHRC imependekeza pia muswada uweke wazi sifa ya wajumbe wa tume kutokuwa na chama cha siasa miaka mitano kabla ya kuteuliwa na Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa ujumuishe kipengele cha kuwapo chombo maalum cha usuluhishi wa migogoro ndani ya vyama.

“Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Ubunge na Madiwani uweke kifungu kinachotoa haki kwa Watanzania waishio nje ya nchi kuwa na haki ya kupiga kura kwa utaratibu am bao sheria itaweka.” alisema Dkt. Henga

Dkt. Henga amebainisha kuwa marekebisho mengine ambayo yanapswa kufanyika kwenye Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni kuhusu watumishi wa umma kuendelea kuwa sehemu ya tume, na tume hiyo kuendelea kutegemea bajeti ya serikali, tume kushauriana na waziri mwenye dhamana na masuala ya utumishi kuandaa muundo wa utumishi wa sekretarieti ya tume.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 21 cha muswada, Tume itaendelea kutumia watumishi wa umma kuwa wasimamizi wa uchaguzi, kwa lugha nyingine, wakurugenzi wa halmashauri, watendaji wa kata, walimu na watumishi wengine wa serikali wataendelea kuwa sehemu ya wasimamizi wa uchaguzi ingawa neno lililotumika ni kuazima."
  
“Kifungu hiki pia kinakiuka uamuzi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu katika shauri la LHRC na Bob Chacha Wangwe, dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Dkt. Henga.

Hata hivyo akizungumza kuhusu ujumuishaji wa wanawake na watu wenye ulemavu katika nafasi mbalimbali za uongozi Dkt. Henga amesema muswada umependekeza kuongezwa kwa kifungu kipya cha 10C (1) (b) (c) kinachoweka takwa la lazima kwa vyama vya siasa kuwa sera ya ujumuishaji wanawake na watu wenye ulemavu katika katika nafasi za uongozi.

Dkt. Henga ameongeza kuwa kifungu hiki bado hakijaweka wazi utaratibu wa namna gani chama kitakachoshindwa kukidhi mahitaji ya kifungu cha 10 C kitawajibishwa kwani kifungu hicho kinaishia kuweka takwa na kuwa sera ya jinsia pekee na hakiweki misingi ya uwajibikai kwa vyama vitakavyoshindwa kutekeleza takwa hilo.

Takwimu zinaonyesha kuwa ushiriki wa wanawake katika nafasi za ubunge umekuwa ukipanda na kusua sua  ambapo kupanda na kusua sua kwa takwimu hizo kunatajwa kutokana na kukosekana kwa mifumo na sera madhubuti zinazoweka mazingira rafiki ya ushiriki wa wanawake katika siasa.

"LHRC inapendekeza kurekebishwa kwa kifungu 10C mswada ili kukiongezea makali na namna vyama vya siasa vitakavyoshindwa kukidhi mahitaji ya kijinsia kuchukuliwa hatua na kuwajibishwa" aliongeza Dkt. Henga.

Mbali na hayo LHRC imependekeza na kuishauri serikali kupitia vikao vya Bunge la mwezi February 2024 iwasilishe mswada wa sheria itakayosimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa tofauti na ilivyo sasa ambapo Wizara ya TAMISEMI ndiyo chombo chenye jukumu hilo.