Jumanne , 14th Nov , 2023

Kufuatia kifo cha mjamzito na kichanga chake kilichotokea Handeni Tanga November 11,2023 katika Kituo cha Afya Kabuku Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu @ummymwalimu amesema tayari Watumishi watatu wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi.

Ummy amesema “Tayari Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba ametuma Timu kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa inayojumuisha Madaktari bingwa wawili (Daktari Bingwa wa Wanawake na Uzazi na Daktari Bingwa wa Huduma za Usingizi ) ili kufanya uchunguzi wa tukio hili”

“Pili, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni amewasimamisha kazi Watumishi watatu walioshiriki kumpatia huduma Mama huyo tangu alipopokelewa Kituoni hadi umauti ulipomkuta ili kupisha uchunguzi wa tukio hili baya na lisilopaswa kuvumiliwa!”

“Tatu, tuhuma hizi pia tayari zimeshapokelewa na Mabaraza ya kitaaluma (Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) na Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania (TNMC)) na vyombo vingine vya dola kwa ajili ya uchunguzi zaidi, hivyo ninaelekeza MCT na TNMC ndani ya Siku 7 kuanzia leo kuniletea taarifa ya uchunguzi wa tukio hili" amesema Waziri Ummy Mwalimu