Jumatatu , 23rd Oct , 2023

Matumizi sahihi na salama ya mifumo ya kieletroniki serikalini, yametajwa kuwa suluhisho la kudumu katika kuziba mianya ya upotevu wa rasilimali za serikali ikiwemo mapato yatokanayo na vyanzo mbalimbali nchini.

Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba, wakati akipokea na kuzindua Mfumo wa Kieletroni wa Kuratibu Ununuzi wa Mafuta Serikalini, ujulikanao kama 'GPSA Intergrated Management Information System' (GIMIS), kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene.

Alisema kuwa, matumizi ya mifumo imara ya kielektroniki yanasaidia kuondoa mianya ya upotevu wa rasilimali za Serikali na kudhibiti watumishi wasio waadilifu, kwa kuwa malipo yote ya serikali yatalipwa kupitia njia sahihi na salama katika taasisi husika.

"Tukifanya kazi kupitia mifumo ya kielektroniki tunapunguza makosa mengi ya kibinadamu, hivyo matumizi sahihi ya mifumo hii yatatuwezesha kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wetu ikiwa ni pamoja na eneo la ukusanyaji wa mapato mbalimbali ya serikali," amefafanua Waziri Nchemba

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, amesema kuwa, lengo la mfumo huo ni kurahisisha utendaji kazi wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), katika uuzaji wa mafuta Serikalini, ili kuweka uwazi na kutunza kumbukumbu za matumizi ya mafuta katika kila taasisi ya umma.

Alisema kuwa, hadi sasa zaidi ya taasisi nunuzi 7070 zinatumia mfumo huo ambapo, taarifa za matumizi ya mafuta kwa kila taasisi zinatunzwa katika mfumo huo na kusaidia katika uandaaji na usimamizi wa mipango ya bajeti ya ofisi, pamoja na udhibiti wa matumizi sahihi ya mafuta kwa taasisi za umma.

Mfumo wa GIMIS umesanifiwa na kujengwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kwa kushirikiana na Ofisi ya Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA).