
Lori lililopata ajali
Akizungumza Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe Theopista Mallya, amewataja waliofariki kuwa ni Levy Simkoko(30)aliyekuwa mzee wa kanisa kutoka Ushirika wa Mbuga na Hosiana Gavu (21)ambaye ni mtoto wa mchungaji.
Kamanda Theopista amesema chanzo cha ajali ni kutokana na kutokea hitilafu kwenye mfumo wa breki na baadaye ya kupasuka bomba mbili za upepo hali iliyosababisha gari kwenda kwa kasi na juhudi za dereva zikashindikana kisha likaanguka na kupinduka na kusababisha vifo vya watu viwili na majeruhi wawili ambao wametibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Kamanda amesema kuwa hilo lori lilikuwa na watu 12 ambao walikuwa wanamsindikiza mchungaji Emmanuel Gavu aliyehamishwa kutoka ushirika wa Mbuga kwenda ushirika wa Msangano.
Mwenyekiti wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Mbozi Mchungaji Laurence Nzowa ambaye yupo safarini Jimbo la Rukwa amesema uhamisho huo ni wa kawaida na ametoa pole kwa familia na Kanisa kwa ujumla.
Katibu wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Mbozi Mchungaji Rayson Kibona amesema baada ya kupata taarifa ya ajali walifika eneo la tukio na kuwafikisha majeruhi hospitali.
Katibu amesema msiba huo ni pigo kwa kanisa na ametoa pole kwa familia na waumini wote wa Kanisa la Moravian Tanzania sanjari na kuwashukuru wale wote walifanikisha hatua zote mpaka mazishi.