Ijumaa , 27th Feb , 2015

VYAMA vya Watu wenye ulemavu nchini, wanakusudia kuishitaki serikali kwenye vyombo vya kimataifa, endapo mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) yataendelea.

Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Wakili Amon Anastaz.

Akizungumza leo kwenye warsha ya ujumuishaji wa watu wenye ulemavu, katika nyanja za maendeleo iliyowezeshwa na EDAN ambayo ni programu ya Jumuiya ya Makanisa Duniani, Mshauri wa mradi wa watu wenye ulemavu, kuhusu haki na maendeleo yao, Dk. Elly Macha amesema Tanzania imesaini mkataba wa kutetea haki za watu wenye ulemavu, lakini imeshindwa kuwalinda na matokeo yake wanauawa ovyo.

Amesema kuwa hali ya mauaji ikiendelea kuwa kama ilivyo sasa, wataelewa wazi kuwa serikali imewaacha peke yao na watalazimika kwenda kwenye vyombo vya kimataifa kuishtaki serikali kwa kushindwa kuheshimu mkataba huo.

Aidha amesema kuwa mbali na hilo katika warsha hiyo wamekubaliana na kutoa wito kwa serikali kusimamia, kuelekeza, kutekeleza na kufuatilia ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika nyanja za maendeleo hususani, kuhakikisha sera, sheria, mipango na upatikanaji wa rasilimali unawezesha ujumuishaji wa masuala hayo.

Dk. Elly amesema kupitia warsha hiyo wametoa tamko la kulaani mauaji ya kinyama ya Albino yanayoendelea kutekelezwa kwa kasi, hasa kanda ya ziwa na kuitaka serikali kuchukua hatua madhubuti kukomesha tatizo hilo.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Felician Mkude, amesema kuna kesi nyingi zimeamuliwa na wengine wamehukumiwa kunyongwa, ila mpaka sasa hakuna aliyenyongwa wapo magerezani,hivyo wanaomba hukumu ikitolewa izingatiwe, kwani isionee huruma wahusika hao wanaoua wenzao kama wanyama.