Jumatano , 11th Oct , 2023

Waziri wa Madini Anthony Mavunde, amemaliza mgogoro wa wachimbaji wadogo wa madini uliodumu kwa mwaka mmoja katika Kitongoji cha Mafurungu, wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Waziri wa Madini Anthony Mavunde

Akizungumza katika mkutano na wachimbaji wadogo hao,Waziri Mavunde amesema kuwa serikali kupitia wizara yake inatambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo katika ukuaji wa uchumi wa Taifa hivyo inafanya kila juhudi ili kuona wachimbaji wadogo wa madini wapo katika mazingira salama ya uchimbaji.

Waziri Mavunde amefafanua kuwa maana ya mazingira bora ya uchimbaji ni pamoja usalama katika uchimbaji, kuchimba kwa kutumia vifaa vya kisasa lakini pia kuwa na taarifa sahihi za uwepo wa madini ili kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha.

Mavunde ameeleza kuwa kutokana na umuhimu wenu katika sekta ya madini leo tunafunga rasmi mgogoro  kwa kuwapatia leseni nne za uchimbaji ili kila mmoja achimbe  bila kuwepo na mgogoro wowote  katika kitongoji cha Mafurungu.

Sambamba na hapo Mhe.Mavunde ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji  katika maeneo yao ya kazi ambapo katika juhudi za kuunga mkono maendeleo ya kitongoji cha Mafurungu  tayari ametoa ahadi ya mifuko 200 ya Saruji na kuwa Balozi wa kujitolea kwa eneo hilo.

Naye, Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahm Mwanga ameupongeza uongozi wa Wachimbaji Wadogo wa madini kupitia Chama Cha Wachimbaji Wadogo Mafurungu (UWAWAMA) kwa kukubali na kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri wa Madini na kuweza kufuta  sintofahamu zote zilizokuwepo awali.