Jumatatu , 2nd Oct , 2023

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amesema kuwa Wizara ya Nishati inafanya jitihada mbalimbali ili kupunguza makali ya umeme nchini na hivyo kuwaondolea wananchi matatizo ya umeme wanayoyapata kwa sasa.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko

Amesema hayo leo Oktoba 2, 2023, baada ya kuwasha umeme katika Kijiji cha Nyanguku na Bunegezi wilayani Geita, mkoa wa Geita ambapo pia alizungumza na wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya maji na barabara katika vijiji hivyo.

"Tumekubaliana, Katibu Mkuu na watendaji wakuu wa taasisi warudi Dodoma kushughulia masuala ya mgawo wa umeme, tunataka tupunguze mgao huu kwa kasi kubwa ili wananchi wasipate matatizo ya umeme, vilevile Naibu Waziri wa  Nishati, Judith Kapinga  anatembelea vituo vya kufua umeme, alianzia Ubungo, ameenda Tegeta na maeneo mengine, lengo letu ni lile, kupunguza makali ya mgawo wa umeme kwa watu wetu," amesema Waziri Biteko

Ameeleza kuwa, Wizara ya Nishati inalitekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan la kushughulikia changamoto za upatikanaji umeme wa uhakika ndani ya miezi sita ili wananchi waweze kufanya shughuli zao bila matatizo.

Kuhusu umeme vijijini amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inataka umeme uwafikie wananchi wote na kwa Mkoa wa Geita imetoa shilingi bilioni 39 kwa ajili ya usambazaji umeme vijijini mkoani humo na dhamira ya serikali ni kufikisha umeme kaya kwa kaya.