Jumamosi , 9th Sep , 2023

Serikali ya Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu (DSFA) zinatarajia kuvuna takribani Dola Milioni 2.1 kupitia mauzo ya leseni 45 za uvuvi wa bahari kuu zilizonunuliwa na wawekezaji kutoka nchi za China na Hispania.

Akizungumza katika hafla ya kusaini mikataba ya mauzo ya leseni hizo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amesema kuwa eneo la bahari kuu kwa upande wa Tanzania bara na Zanzibar lina ukubwa wa takribani kilomita za mraba 220,000 ambazo kwa muda mrefu zimekuwa hazitumiki ipasavyo.

“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana imani kubwa sana kwetu hivyo ni lazima tuwe wabunifu katika utekelezaji wa maelekezo yake ambayo amekuwa akitutaka tuhakikishe rasilimali hii ya maji ya bahari inatumika kikamilifu kuwanufaisha Watanzania wote” Amesema Mhe. Ulega.

Aidha, Ulega amebainisha kuwa eneo la bahari linalomilikiwa na Tanzania bara na Zanzibar lina uwezo wa kuhimili mpaka meli 100 hivyo ametoa rai kwa wawekezaji wengine wenye nia ya kuwekeza kwenye Uvuvi wa bahari kuu kufanya hivyo ambapo amewahakikishia hali ya usalama na mazingira rafiki ya kufanya shughuli zao wakati wote

Kwa upande wake Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi kutoka Zanzibar, Mhe. Suleiman Makame amewahakikishia wawekezaji hao kuwa Wizara yake kupitia mamlaka ya usimamizi wa Uvuvi wa bahari kuu (DSFA) itasimamia na kutekeleza vipengele vyote vilivyopo kwenye leseni hizo.

Hatua hiyo ni miongoni mwa jitihada zinazochukuliwa na  Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha eneo la bahari kuu linatumika vizuri ili kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni hapa nchini.