Jumatano , 6th Sep , 2023

Wanafunzi zaidi ya 100 kutoka katika Kata tatu za Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wamepatiwa mbinu za kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia pamoja na madhara ya mimba na ndoa za utotoni na kuwataka kuwa mabalozi wa kupinga vitendo hivyo.

Kutokana na changamoto ya matukio ya ukatili wa kijinsia kuendelea kutokea katika maeneo mbalimbali na kukatisha ndoto za watoto wa kike kufikia malengo yao,elimu imeanza kutolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi ili kutokomeza vitendo hivyo.

Nao baadhi ya wanafunzi wamesema elimu waliyoipata itawawezesha kwenda kuwa mabalozi wazuri wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wanafunzi wengine. 

Mwanafunzi mwingine Loveness Ally amesema baadhi ya watoto wa kike wamekuwa wakipewa vitisho na wazazi wao ili waolewe katika umri mdogo jambo ambalo limekuwa likikatisha ndoto za wanafunzi na wengine kufanyiwa ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wake mshauri  mwelekezi wa mradi wa kupinga ndoa za utotoni   unaotekelezwa na Tume ya taifa ya UNESCO Dk Rehema Horera amesema bado kuna changamoto ya ndoa na mimba za utotoni katika Mkoa wa Shinyanga.

Amesema wanafunzi wa kike wa shule za msingi  ni miongoni mwa walengwa wa program  hiyo  ya kuwaanda wanafunzi kuwa mabalozi  katika uhamasishaji kuhusu madhara ya ndoa za utotoni.

Afisa program kutoka Unesco Godluck Patrice amesema lengo ni kuwaandaa mabinti kuwa mabalozi wazuri wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuhakikisha wanakuwa katika mazingira salama.

Afisa elimu maalum Halmshauri ya Shinyanga Irene Kisweka amesema wanafunzi hao wamewezeshwa kujua njia sahihi za kufikisha taarifa pindi wanapofanyiwa ukatili. 

Naye Mwalimu kutoka Kata ya Ilola Peter Edward amesema mafunzo na mbinu walizopatiwa wanafunzi zitawawezesha kuwa mabalo wazuri wa kutokomesha ukatili wa kijinsia.

Wanafunzi waliojengewa uwezo na Tume ya taifa ya UNESCO ni kutoka Kata ya Ilola,Iselamagazi na Lyabukande ili kuwaandaa kuwa mabalozi wa kupinga ukatili wa kijinsia.