Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile
Balile ametoa kauli hiyo tarehe 17 Agosti 2023, alipozumgumza na baadhi ya wanahabari katika ofisi za jukwaa hilo, jijini Dar es Salaam.
Alisema, mwenye jukumu la kusimamia na kukamilika kwa kanuni ni Waziri wa Habari, Mawasiliano n Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.
"Tungependa kanuni za habari zipatekane mpaka kufika Oktoba, hili ni ombi kwa kuwa, Waziri wa Habari (Nape Nnauye) halazimishwi na sheria kuhusisha wadau, ni kutokana na utaratibu wake wa kushirikisha wadau ndio maana anafanya hivyo, wala safari hii suala la kanuni za habari halipelekwi bungeni, linaishia kwa kwake Waziri Nape," amesema Balile
Balile amesema baada ya bunge kupitisha marekebisho ya sheria ya habari, kinachofuata sasa ni kuomba fursa ya kukutana na serikali kwa ajili ya kupendekeza mambo gani yaingie kwenye kanuni.
Amesema miongoni mwa mambo ambayo wadau wa habari wangependa kuona yanaingia kwenye kanuni mpya na kuanza kutumika ni pamoja na suala la leseni ya magazeti kuwa zaidi ya miaka mitano tofauti na ilivyo sasa.
"Tutashauri serikali kwamba, kanuni zetu zielekeza kuwa leseni pamoja na kitambulisho cha mwanahabari (press card), zidumu kwa zaidi ya miaka mitano," ameongeza Balile
Kwenye mkutano wake na wanahabari Balile alisema, eneo lingine wanalotarajia liingie kwenye kanuni, ni umiliki wa hisa katika vyombo vya habari kutowekewa mipaka.