
Wananchi kote nchini wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya homa ya ini ikiwa ni pamoja na kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa homa hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama Julai 28, 2025 katika maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani mkoani Ruvuma na kuongeza kuwa Serikali ya awamu ya Sita inaendelea na juhudi za utoaji wa huduma tiba na kinga dhidi ya Homa ya Ini, huku huduma za upimaji na matibabu zikipatikana kwenye Hospitali zote za Rufaa za Mikoa, Kanda na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Waziri Mhagama amebainisha kuwa kupungua kwa maambukizi ya Homa ya ini nchini ni juhudi za pamoja kati ya Serikali na Wadau wa Sekta ya Afya waliokwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo wakiwa na lengo la kidunia la kutokomeza ugonjwa huo ifikapo 2030.
Ameongeza kuwa vituo vya huduma za afya kuanzia ngazi ya Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati vitaendelea na utaratibu wa kupima Homa ya Ini na kutoa rufaa kwa huduma za Homa ya hiyo, huku mipango ya Serikali ikiendelea kuviwezesha vituo hivyo kutoa huduma kamili.