Jumapili , 23rd Jul , 2023

Katibu wa Chama cha Wauguzi Mkoa wa Pwani Dafroza Mnzava ameiomba Serikali kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili wauguzi ikiwamo suala la muundo na posho ya mazingira hatarishi na stahiki mbalimbali.

Dafroza   ameyasema hayo leo Jumapili Julai 23, 2023 wakati akisoma risala kwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze

Pia Katibu huyo ameiomba Serikali kuendelea kuajiri wauguzi ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema taaluma ya Uuguzi ni kazi ya uthubutu, utayari pamoja na kujitoa kwa ajili ya kuwahudumia  wenye mahitaji ya kiafya huku akiwataka wauguzi kuendelea kuchapa kazi  kwa weledi na kwa kuzingatia miiko na maadili ya taaluma yao.

Aidha, Mhe. Kikwete amesema Ofisi ya Rais-UTUMISHI inaendelea kuzifanyia kazi changamoto za kimuundo za taaluma hiyo na changamoto nyingine itaishirikisha Wizara husika ya Afya ili ziweze kufanyiwa kazi.
Katika hatua nyingine Kikwete amekubali ombi la kuwa mlezi wa Wauguzi katika Mkoa wa Pwani huku akiahidi kuwapa ushirikiano ili kuwaongezea morali Watumishi hao katika kutekeleza majukumu yao.

‘’Natambua mchango wenu adhimu kwa mustakabali wa afya zetu kwani ziko mikononi mwenu, napenda kuwaahidi mimi kama mlezi wenu niko tayari kuwapa ushirikiano muda wote mtakaponihitaji” Amesisitiza Kikwete.

Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu “WAUGUZI WETU, MUSTAKABALI WA AFYA ZETU” yamefanyika mkoani humo ikiwa ni kuenzi kumbukumbu ya Muasisi wa Uuguzi na Ukunga Duniani, Bi. Florence Nightingale wa nchini Italia aliyejitoa kwa moyo kuwahudumua wenye mahitaji ya kiafya