Jumapili , 23rd Jul , 2023

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya Kenya (DCI) imeanza msako wa kuwasaka washukiwa wanaoaminika kuzika miili mipya katika msitu wa Shakahola.

Chanzo katika DCI kilichozungumza na chombo kimoja  cha habari cha Kenya kimeeleza kuwa shirika hilo lilipokea taarifa kutoka kwa maafisa waliotekeleza shughuli ya ufukuaji kuwa miili mipya iligunduliwa msituni na ikidaiwa kuzikwa mwezi mmoja uliopita

Kurugenzi ilipitia ushahidi huo na kutuma mara moja timu ya wachunguzi waliofunzwa na waliobobea kuchukua jukumu hilo. Ripoti za polisi zilionesha kuwa maafisa hao walipata makaburi ya kina kirefu yenye miili mipya msituni ambayo ilifukuliwa na kuhifadhiwa kwa uchunguzi zaidi na mashirika ya serikali.

Kutokana na hali hiyo, DCI sasa wanauomba umma  taarifa zinazoweza kupelekea kukamatwa kwa washukiwa hao. Pia walimwomba mtu yeyote ambaye huenda ameona chochote cha kutiliwa shaka katika Msitu wa Shakahola kujitokeza.

"DCI imejitolea kuwafikisha washukiwa mahakamani na kuwalinda wananchi dhidi ya madhara. Tunaomba usaidizi wako kuhakikisha hilo linafanyika," Kilisema chanzo hicho.

Katika juhudi hizo, maofisa hao wa Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai pia wameanzisha upya uchunguzi wa dhehebu la Paul Mackenzie ambalo limekuwa likilalamikiwa kwa ‘kuwavuruga’ ubongo wafuasi wake na kuwalazimisha kujiua kwa njaa na kuishi maisha duni.

Idadi ya waliofariki katika madhehebu ya Shakahola ilifikia 403 baada ya miili 12 zaidi kufukuliwa mnamo Jumatatu Julai 17 kutoka kwenye ardhi inayohusishwa kumilikiwa na mchungaji Paul Mackenzie. Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Rhoda Onyancha, alithibitisha rasmi ukusanyaji wa sampuli za DNA 257 kusaidia uchunguzi, huku idadi ya waliookolewa ikifikia 95.