Ijumaa , 21st Jul , 2023

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga anasema homa ya mafua  imemzuia kushiriki maandamano ya siku tatu mitaani ambayo yanapinga  gharama za maisha na ongezeko la kodi.

"Sio lazima viongozi wa upinzani waonekane mitaani," Bw Odinga aliambia kituo kimoja cha televisheni cha Kenya kuhusu maandamano hayo ambayo yanatarajiwa kumalizika leo.

Mwanasiasa huyo mkongwe, ambaye alishindwa katika uchaguzi wa rais uliokumbwa na utata mwaka jana, alisema maandamano ya  kubadilisha hali ya mambo  ni ya watu na hayakuwa yake peke yake.

Alikanusha madai kwamba kutokuwepo kwake ni njama ya kufanya makubaliano na Rais William Ruto na kuongeza kuwa hataki kuwa sehemu ya serikali.

"Hatujafanya hivyo, na hatutatafuta 'handshake arrangement'," kiongozi huyo wa upinzani alisema akirejelea jina la makubaliano aliyofanya na Rais aliyepita, Uhuru Kenyatta.

Kwa upande wake Rais Ruto amesisitiza kuwa hatashiriki katika majadiliano na Bw Odinga ili kutatua mkwamo uliopo. Siku ya Alhamisi, alipongeza hatua ya polisi  mkuu wa polisi alisema maandamano hayo yalikuwa tishio kwa usalama wa taifa na kuwatuma maafisa wa kutuliza ghasia kote nchini.