Alhamisi , 20th Jul , 2023

Jeshi la polisi mkoa wa Tanga linawashikilia watu 11 waliokuwa wameweka kambi jijini Tanga na kuendesha wizi kwa njia ya mtandao katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo ya Kanda ya Kaskazini. 

Kamanda wa Polisi mkoa Tanga Henry Mwaibambe

Watuhumiwa hao wamekuwa wakituma ujumbe mfupi wa maneno na namba za simu kwa watu mbalimbali wa kuomba kutumiwa pesa. 

Kamanda wa Polisi mkoa Tanga Henry Mwaibambe, ameeleza kuwa aina ya utapeli waliobainika kuutumia watuhumiwa hao baada ya kuwahoji wamesema kuwa walikuwa wakimtaka mwenye simu kutuma fedha na wengine kuomba namba za siri. 

Kamanda Mwaibambe amesema watuhumiwa hao walikuwa wamepanga nyumba katika eneo la  Donge jijini Tanga na kulipa kodi ya mwezi mmoja na kulipia shilingi laki nane ili waweze kukamilisha utapeli wao ambapo wamekutwa na simu, laini za simu 42 ,jiko na chotezo kwa ajili ya kuchomea line na karatasi zenye orodha za namba walizokwishatapeli na wanazotarajia kuendesha utapeli huo pamoja na fedha shilingi za Tanzania, Dola za Marekani na fedha za Congo DRC.

Watuhumiwa hao walikutwa pia na kadi za simu za mitandao mbalimbali, pikipiki, kadi za benki 5, simu ndogo za tochi 13 za aina mbalimbali, simu 11 kubwa za smartphone.

Kamanda Mwaibambe amewataja waliokamatwa na kuhusishwa na utapeli huo kuwa ni Hadija Nyange (34) mkazi wa Muheza, Zaina Athumani (25) mkazi wa Mwanzange,Innocent Omeme (35) wa Dar es salaam,Abdulaziz Nzori (31) wa Dar es Salaam, Said Hassan (24) wa Dar es Salaam, Rashid Habibu (23) wa Dar es Salaam,Said Juma (30) ,Idd Kaniki (35),David Rupiana wa Dar es Salaam (22),Omary Mohamed (27) wa Mkanyageni Tanga na Salum Rajab (24) wa Dar es Salaam.