Jumanne , 27th Jun , 2023

Jeshi la Polisi mkoa wa Iringa limepokea msaada wa pikipiki 10 za kisasa zenye thamani ya shilingi milioni 55 pamoja na  jengo la kantini yenye thamani ya shilingi milioni 45 kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani humo.

Pikipiki zilizokabidhhiwa kwa Jeshi la Polisi Iringa

Akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano Mkuu wa mkoa wa iringa  Halima Dendego amewapongeza wadau kutoka sekta binafsi kwa kutoa vifaa vya usafiri kama sehemu ya kupanua wigo wa mapambano dhidi ya vitendo vya uhalifu pamoja na kurudisha fadhila kwa jamii

Kwa upande wao baadhi ya wadau waliofanikisha zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kampuni ya Asas, East African Bornwood, Yisen International Investment, wamesema kuwa lengo la kutoa mchango huo ni kuongeza ufanisi wa kazi zinazofanywa na jeshi hilo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi, amesema kuwa kwa sasa wanaendelea na zoezi la utoaji mafunzo kwa askari watakaotumia pikipiki hizo ili kutambua matumizi sahihi na utunzaji wa vyombo hivyo vya moto