
Ramaphosa ameweka wazi nukta 10 za mpango wa amani wa Afrika ambao unatafuta makubaliano ya hatua za kujenga amani hata kama Ukraine wiki iliyopita ilianza mashambulizi ya kukabiliana na kuvirudisha nyuma vikosi vya Urusi
"Vita hivi lazima viwe na mwisho, lazima vitatuliwe kwa njia ya mazungumzo na kidiplomasia," Amesema Ramaphosa akiwa huko St Petersburg Jumamosi .
Wataalamu wa siasa za kimataifa wanasema Ujumbe huu una umuhimu maalum kwa Afrika ambayo inategemea usambazaji wa chakula na mbolea kutoka Urusi na Ukraine. Vita hivyo vimezuia uletaji wa bidhaa za ngano ambayo huzalishwa kwa wingi na nchi hizo mbili.
Putin alikatiza hotuba ya ufunguzi ya viongozi wa Afrika wanaotaka kupatanisha mzozo huo ili kutoa sababu kwa nini aliamini mapendekezo yao mengi yalikuwa potofu.Alisisitiza msimamo wake kuwa Ukraine na nchi za Magharibi zilianzisha mzozo muda mrefu kabla ya Urusi kutuma vikosi vyake vya kijeshi kwenye mpaka mwezi Februari mwaka jana. Alisema Urusi haijawahi kukataa mazungumzo na upande wa Ukraine, ambao ulikuwa umezuiwa na Kyiv.
Licha ya ujumbe huo wa Afrika katika nchi mbili zinazohasimiana, wataalamu wa siasa za kikanda wanaona kuwa nafasi ya mazungumzo ya amani bado ni finyu huku Ukraine na Urusi zikichukua misimamo tofauti kabisa.
Ukraine inaitaka Urusi iondoe wanajeshi wake katika maeneo yake yote inayokalia kama sharti la mazungumzo ya amani. Kremlin kwa upande wake, inataka Ukraine itambue Rasi ya Crimea ambayo Moscow ilinyakua kinyume cha sheria kutoka kwa Ukraine mwaka 2014 kama sehemu ya Urusi na kutambua mafanikio mengine ya ardhi ambayo imepata.