Alhamisi , 8th Jun , 2023

Baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe, kudai kuwa kama kweli mkataba wa DP World na Tanzania una manufaa makubwa kwa nchi, kwa nini bandari za Zanzibar hazimo kwenye mkataba huu?

Bandari ya Zanzibar na Dar es Salaam

Imeelezwa kuwa uchukuzi siyo sekta ya muungano. Ndiyo maana, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inasimamia bandari za Tanzania bara na Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) inasimamia bandari za Zanzibar.

Aidha, Tanzania bara kuna Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) nayo ina Wizara yake ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi. 

Mkataba wa DP World a Tanzania unahusisha kuendeleza bandari za Tanzania bara, ndiyo maana bandari za Zanzibar hazijatajwa, kwani SMZ na ZPC zina mipango yake inayo jitegemea ya kuendeleza bandari za Zanzibar.

Aidha kuhusu Mbowe kuhoji Uzanzibari wa Rais Samia Suluhu Hassan na Prof. Makame Mbarawa kwenye mjadala wa DP World umejibiwa kuwa, labda Mbowe amesahau kuwa hii ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mtanzania yoyote kutoka pande yoyote ya Muungano, kanda yoyote au kabila lolote ana haki ya kuwa kiongozi wa nchi na kufanya maamuzi kwa uzalendo kwa maslahi ya pande zote mbili za Muungano.

Tunu hii ya Umoja tuliachiwa na waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume.

Tangu alipoingia madarakani, Rais Samia ameonesha uzalendo mkubwa kwa kufungua nchi na kuongoza siasa mpya za maridhiano na uvumilivu, huku akipanua uwanja wa uhuru, haki na demokrasia.

Kwa kuhoji Uzanzibari wa Rais na Waziri wa Uchukuzi kwenye mjadala wa mkataba wa DP World, Mbowe amekusudia kupandikiza chuki, uhasama na mfarakano kati ya Tanzania bara na Zanzibar ili kuligawa taifa.

Kiongozi bora huunganisha na kuliponya taifa. Siyo kuligawa taifa na kulirejesha kwenye siasa za chuki, uhasama na mfarakano.

Hatutakubali kutenganishwa kama taifa na kupandikizwa chuki kati ya pande zetu za muungano na tofauti ya itikadi. Never, never and never again!