Alhamisi , 8th Jun , 2023

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amesema watawatumia Kaimu Sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam, Walid Alhad Omar na Mchungaji Boniface Mwamposa kuwa mabalozi wa uhifadhi wa Bahari ili wasaidiane nao katika kuelimisha jamii zinazoishi kando ya Bahari juu ya athari ya uuvuvi haramu.

Katika picha ni Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango, Waziri wa Mifugo Abdallah Ulega na Naibu wake David Silinde, viongozi wengine pamoja na mabalozi wa ubifadhi Bahari, Sheikh Walid Alhad Omar na Mchungaji Mwamposa

Waziri Ulega alisema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hii leo Juni 8, 2023.

Alifafanua kuwa pamoja na uwepo wa sheria  kwenye usimamizi na uendelevu wa rasilimali za Bahari, ni muhimu pia kushirikiana na jamii katika kuhakikisha mazingira ya Bahari yanahifadhiwa vizuri kwa maslahi ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Waziri Ulega amesema kwa kutambua umuhimu wa kushirikisha jamii wameamua kuwatumia viongozi hao wa dini kuwa mabalozi na kuwaelimisha waumini wao juu ya umuhimu wa kuepuka vitendo ambavyo vinapelekea uharibifu wa mazingira ya Bahari.

Naye, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, David Silinde amesema kuwa pamoja na changamoto ya matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo imekuwa moja ya kisababishi cha uharibifu wa mazingira ya bahari, yeye pamoja na Waziri Ulega wamedhamiria kuhakikisha kuwa wanaendelea kusimamia  matumizi endelevu ya rasilimali za Bahari ili ziendelee kuchangia vyema kwenye uchumi wa buluu.

Kiongozi mwingine wa dini atakayeshiriki kuelimisha jamii ni kutoka Kanisa Katoliki Tanzania, Padri James Ngonyani.

Kauli Mbiu ya Siku ya Bahari Duniani kwa mwaka 2023 ni “Sayari ya Bahari: Mawimbi Yanabadilika”.