Naibu Waziri Pinda ameyasema hayo wakati alipofanya ziara mkoani Katavi ya uzinduzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Mlele tarehe 24 Machi 2023.
Kauli hiyo imeibuka wakati Naibu Waziri Pinda alipokutana na Bw. Peter Lukas mkazi wa Mpanda ambaye anashitakiana na mwenzake kwa kesi ambayo inaweza kutatuliwa kwa kukubaliana bila kufungua kesi rasmi katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya.
"Kesi nyingine ni ndogondogo sana na zinahitaji tu kauli za watu wawili lakini mtu anazunguka nayo hiyo kesi ya ekari moja miaka kumi mpaka mashitaka yanaibuka, kumbe kama mngekuwa na uwezo wa kukubaliana mkakaa pamoja mgeweza kuelewana bila hata kufika katika Mabaraza ya Ardhi ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya" amesema Mhe. Pinda.
Katika kusisitiza hilo Mhe. Pinda ameongeza kuwa wananchi wanatakiwa kuepuka mashitaka ya mara kwa mara kwa sababu kuendesha kesi ni gharama kubwa sana hasa katika kutafuta ushahidi, mawakili na hata katika kuisimamia mpaka kupatikana hukumu yake.
"Hizi kesi zina gharama kubwa sana, wewe unatoka Halmashauri ya Mpimbwe unakwenda Mpanda kwa ajili ya kesi ambayo sio ya lazima ukizingatia wewe mwenyewe unajigharimia, mashahidi unagharimia, kulala gharama, yaani utaratibu mzima unazidi kesi uliyopeleka mahakamani“ Ameongeza
Katika ziara hiyo ya mkoani Katavi Naibu Waziri Pinda amekutana na watumishi wa sekta ya ardhi, mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya pamoja na kukutana na watumishi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambapo amepokea taarifa za utendaji kazi pamoja na kutoa maelekezo.
Aidha, Mhe. Pinda pamoja na kuzindua Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ya Mlele amekagua Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Mpanda na kukagua ujenzi wa Nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) za wilaya ya Mlele mkoani Katavi.
Mkoa wa Katavi ni wa tatu kutembelewa na Naibu Waziri Pinda tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 26 Februari 2023 kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akitokea Wizara ya Katiba na Sheria.
Mara tu baada ya kuteuliwa kutumikia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maeneleo ya Makazi Naibu Waziri Pinda amefanya ziara Mkoani Arusha na Dar es salaam ambapo amekutana na Watumishi wa Sekta ya Ardhi ili kupokea taarifa za utendaji kazi pamoja na kutoa maelekezo ya Serikali.