Jumapili , 15th Feb , 2015

Timu ya Simba ya jijini Dar es salaam imeisambaratisha timu ya Polisi Morogoro kwa kuichapa mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara.

Mabao ya Simba yamefungwa na Ibrahim Hajib dakika ya 14 na Eliasi Maguli dakika ya 63.

Katika mchezo wa leo Simba walionekana kuwa na uhai zaidi ikilinganishwa na mechi zilizopita, kwa kucheza kwa nguvu katika dakika zote 90 huku ikishangiliwa na mashabiki wake waliosafiri kutoka Dar es salaam hadi Morogoro kwa ajili ya kuipa nguvu timu hiyo ambayo imekuwa na mwenendo wa kusuasua.

Katika mchezo wa mzunguko wa Kwanza uliopigwa Taifa mwaka jana, timu hizi zilitoka sare ya mabao 2-2.

Katika mechi nyingine ya Ligi Kuu iliyopigwa leo, Kagera Sugar imeendelea kutesa katika makazi mapya baada ya kuichapa JKT Ruvu Stars bao 1-0 katika dimba la CCM Kambarage mjini Shinyanga bao likifungwa na Atupele Green dakika ya 31.

Huu ni mchezo wa pili mfululizo kwa Kagera kupata ushindi tangu ihamie katika uwanja huo kama uwanja wake wa nyumbani baada ya kuukimbia ule wa CCM Kirumba Mwanza ambako ilipoteza mechi 3 mfululizo.

Kwa matokeo haya, Simba imepanda hadi nafasi ya 4 kwa kufikisha point 20, ikiwa nyuma ya Kagera Sugar ambayo nayo imepanda hadi nafasi ya 3 ikiwa imefikisha point 21.

Polisi Morogoro na JKT Ruvu Stars zimeshuka hadi nafasi ya 6 na 7 chini ya Mtibwa Sugar zote tatu zikiwa zimebaki na point 19 kila moja.