Mwanasheria mkuu wa serikali Mh. George Masaju amesema mahakama ya kadhi itakayoanzishwa kisheria haitahudumiwa na serikali na itakuwa ya hiari kwa waumini wa dini ya kiislamu watakaoiridhia katika masuala ya ndoa, talaka, mirathi pamoja na wakfu na kutaka wanasiasa kuacha kukuza mijadala ya suala hilo kwa maslahi yao binafsi.
Akizungumza katika mahojiano maalum na vyombo vya habari vya IPP Bw.Masaju amesema uwepo wa mahakama hiyo utaisaidia serikali katika kuipunguzia mzigo wa mlundikano wa kesi uliopo hivi sasa hivyo ni bora dini zote zikaiunga mkono.
Aidha mwanasheria mkuu huyo wa serikali amekiri madhaifu yaliyofanywa na serikali ya kutotoa elimu kuhusiana na faida ya mahakama ya kadhi kuwa yamechangia pia mjadala kuhusiana na uanzishwaji wake.
Amesema kuwa kuwepo kwa mjadala huo kunalenga kuifanya jamii iache kujadili mambo yanayolikabili taifa, ambayo ni upigaji kura ya maoni ya katiba pendekezwa, uandikishwaji wa wapiga kura pamoja na uchaguzi mkuu amesema.