Ijumaa , 7th Oct , 2022

Naibu Waziri Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Hamad Hassan Chande amesema Mabadiliko ya tabianchi ni halisi na athari zake tayari zinaonekana sio tu katika Mazingira bali pia katika Ukuaji wa uchumi na jamii kwa ujumla.

Naibu Waziri Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Hamad Hassan Chande

Naibu Waziri Chande amesema hayo wakati wa kufunga warsha iliyofanyika kwa muda wa siku nne kuanzia 3-6 Oktoba 2022 katika hotel ya Kibo Palace, jijini Arusha warsha ambayo ilijadili kuhusu upatikanaji wa fedha katika mifuko mbalimbali ya mabadiliko ya tabianchi duniani na maandalizi ya Mkutano wa ishirini na saba wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (cop27)

Ametoa rai kwa washiriki hao kuweka nguvu ya pamoja katika kutafuta rasilimali fedha zitakazowezesha kuwa na ufanisi na tija katika jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika pande zote mbili za Muungano.

“Kwa niaba ya Wizara ya Fedha ninaomba kuahidi kuwa Wizara itandelea kutoa ushirikiano kwa wadau wote ili kuiwezesha nchi yetu kuongeza rasilimali fedha na kuwezesha kunusuru hali za jamii zetu tunazoziongoza” Amesema Naibu Waziri Chande 

Awali Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Omar Shajak amesema katika siku nne za warsha hiyo mijadala mbalimbali juu ya masuala muhimu kama vile kuongeza wigo wa upatikanaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, utekelezaji wa mchango wa Taifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032) zilijadiliwa.