Hii itakuwa ni mara ya pili kwa shirikisho la mpira wa wavu nchini (TAVA) kuchaguliwa kuwa wenyeji wa michuano mikubwa barani Afrika kwa nchi za ukanda wa tano.
Tanzania, katikati ya mwezi ujao Februari 16-18 itakuwa wenyeji wa michuano ya mpira wa wavu kwa nchi za kanda ya 5 Afrika na kwa mujibu wa Rais wa TAVA, Augustino Agapa, wanajiandaa pia kualika timu kwa ajili ya michuano hiyo ya mataifa ya Afrika.
Agapa amesema, uchaguzi wa nchi wenyeji wa michuano hiyo ulifanyika hivi karibuni nchini Misri katika katika mkutano wa marais wa vyama vya wavu kutoka nchi za kanda ya 5.
Timu kutoka nchi za Kenya, Burundi, Somalia, Rwanda, Ethiopia, Djibouti na wenyeji Tanzania zitashiriki michuano hiyo ya wavu ya ufukweni, ambao bingwa atashiriki michuano ya kombe la Afrika (Africa Cup) itakayofanyika Septemba nchini Congo Brazzaville ili kupata timu itakayoshiriki michuano ya Olimpiki mwakani mjini Rio de Janeiro, Brazil.