Jumatano , 7th Jan , 2015

Naibu waziri wa fedha nchini Tanzania Mwigulu Nchemba amesema serikali imewasimamisha kazi watumishi Saba wa wizara hiyo kupisha uchunguzi wa kashfa ya fedha za Akaunti ya Tegeta ESCROW.

Waziri Nchemba ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es salaam alipotembelea Hospitali ya Mwananyamala ambapo alisema fedha hizo zilizotumika kiubadhilifu zingeweza kuokoa maisha ya wagonjwa na hasa watoto

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mwananyamala Dkt. Sophinias Ngonyani amesema upungufu wa majengo katika Hospitali hiyo unasababisha msongamano mkubwa wa wagonjwa katika Hospitali hiyo ambayo kwa siku inapokea wagonjwa zaidi ya 2000.

Nchemba amefanya ziara hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho yake ya kumbukumbu yake ya siku ya kuzaliwa ambapo leo ametimiza umri wa miaka 40.

Wakati huo huo Naibu Waziri Mwigulu Nchemba amesema kwamba bei ya umeme na Gesi itashuka kwa watumiaji wa huduma hiyo nchini Tanzania mara baada ya kukamalika kwa mradi mkubwa wa bomba la Gesi mwezi June mwaka huu.

Ametoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa ikiwa kushuka kwa bei za mafuta katika soka la dunia pia kutasababisha kushuka kwa bei ya nishati ya umeme nchiniTanzania.

Nao Madereva wa Bodaboda, Bajaji na Taxi wamewata maafisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji EWURA kuacha kukaa maofisini na kwenda mitaani kukagua vituo vya kuuzia mafuta kwani kuna baadhi ya vituo vinauza mafuta kwa bei ya juu na kupuuza bei elekezi ambayo ni shilingi 2000.

Wakizungumza na Hotmix baadhi ya madereva jijini Dar es Salaam leo wamesema kuwa maafisa wa EWURA, wawachukulie hatua wamiliki wa vituo vya mafuta wanaokaidi agizo la serikali.