Jumanne , 6th Jan , 2015

Polisi Jijini Dar es Salaam wamelazimika kufyatua risasi hewani na kufyatua mabomu ya machozi kufuatia kuibuka kwa vurugu katika hoteli ya Land Mark Ubungo ambapo shughuli ya uapishaji wa wenyeviti wa serikali Mitaa zilikuwa zinafanyika.

Jeshi la Polisi limelazimika kutumia mabomu ya machozi ili kutawanya baadhi ya wananchi waliovamia zoezi la kuapishwa kwa wenyeviti wa serikali za mitaa katika halmashauri ya manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Vurugu hizo, zinadaiwa kuibuliwa na wafuasi wa vyama vya upinzani kwa madai kuwa Mwenyekiti mmoja wa Chama tawala CCM aliyetaka Kuapishwa hakuwa ameshinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uliofanyika mwezi Desemba mwaka jana.

EATV ilifika katika eneo hilo la Ubungo Riverside na kukuta umati mkubwa wa watu tayari wakifika katika eneo hilo ambapo ili kuruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi ni lazima uoneshe barua ya uthibitisho kutoka kwa watendaji wa kata mbalimbali lengo ikiwa ni kudhibiti watu wasio husika kuingia ndani.

Licha ya kuwepo kwa barua hizo, bado baadhi ya wananchi waliodai wametoka katika mtaa wa Pakacha kata ya Tandale wakaanza malalamiko wakihoji kwanini kiongozi aliyeshinda katika mtaa huo kwa tiketi ya CUF kazuiliwa kuingia ndani na kumruhusu kiongozi wa CCM ambaye hakushinda, hali iliyozua mabishano na kusababisha Polisi kuwaondoa katika eneo hilo.

Baadhi ya wananchi waliojitambulisha kuwa ni wafuasi wa UKAWA, wakaamua kumshambulia mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Msisiri A Bwana Juma Mbena kwa tiketi ya CCM kuwa hakushinda kihalali na badala yake aliyeshinda ni Gasbert Chambembe kwa tiketi ya CUF kwa kura 497, kipigo hicho kilisababisha Bwana Juma Mbena kuingia kwenye karavati ili kuokoa maisha yake.

Ghafla kiongozi mwingine kutoka mtaa wa Ukwamani kata ya Kawe Bwana Sultani Geta kwa tiketi ya CCM akaanza kushambuliwa hali iliyolazimu polisi kutumia mabomu ya machozi kama hivi.

Kabla ya zoezi la kuapishwa kuanza polisi waliendelea kupiga mabomu ya machozi na kusababisha watu kuondoka katika eneo hilo huku baadhi ya watu wakionekana kushikiliwa na jeshi la polisi.

Baada ya kikosi cha kutuliza ghasia FFU kudhibiti vurugu hizo, Zoezi la kuwaapisha viongozi wa serikali za mitaa liliendelea kwa viongozi 152 kuapishw kati ya viongozi 192.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni mhandisi Mussa Natty amewataka viongozi walioapishwa kufanyakazi kwa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kushughulikia matatizo katika maeneo yao bila kujali itikadi za vyama vyao.
Baadhi ya wenyeviti wameahidi kufanya kazi kwa bidii.