Jumatatu , 29th Dec , 2014

Shirika la viwango nchini TBS limefanya ukaguzi wa kushtukiza na kufungia kiwanda cha Devideic Group kinachotengeneza juisi aina ya Into kilichopo Kihonda manispaa ya Morogoro kwa kuuza juice zenye vimelea vya wadudu.

Shirika la viwango nchini TBS limefanya ukaguzi wa kushtukiza na kufungia kiwanda cha Devideic Group kinachotengeneza juisi aina ya Into kilichopo Kihonda manispaa ya Morogoro kwa kuuza juice zenye vimelea vya wadudu ambazo hazifai kwa matumzi ya binadamu na kuagiza juice hizo kuondolewa sokoni mara moja.

Akizungumza wakati wa kufunga kiwanda hicho afisa viwango TBS Raurence Chenge amesema TBS limefunga kiwanda hicho baada ya kubaini kuwa juisi inayozalishwa katika kiwanda hicho zina vimelea vya wadudu na kiwanda hicho kinazalisha chini ya kiwango pamoja na kutumia vikoleza yya sukari kinyume na utaratibu.

Naye afisa uhusiano wa TBS Roida Andusamile amesema sambamba na kuzalisha chini ya kiwango kiwanda hicho hakijatenganishwa na nyumba ya kuishi jambo ambalo ni kinyume na sheria ya viwanda ambapo amewataka wafanyabiashara kuondoa juisi hizo sokoni maramoja na ametoa tahadhari kwa wananchi kuacha kununua juisi aina ya Into kwani hazifai kwa matumizi ya binadamu.

Kwa upande wake meneja uzalishaji wa kiwanda cha Devideic Group Limited Tadeus Ngonyani amesema hajakubaliana na utaratibu uliotumika kufunga kiwanda hicho kwani ameonewa huku akilalamikia kuwa kiwanda chake kinazalisha kwa kufuata taratibu za viwango kama viwanda vingine vinavyotengeneza juisi.