Alhamisi , 18th Dec , 2014

Licha ya serikali kuhamasisha wananchi kujiunga katika vikundi ili waweze kunufaika na mikopo kutoka serikalini na taasisi za kifedha hali imekua tofauti kwa baadhi ya wana vikundi vya Vicoba mkoani Njombe ambao wamesema mkopo haufiki kutoka ban

Rais wa Vicoba Nchini Bi. Devotha Likokola.

Wakizungumza na East Africa Radio kwa nyakati tofauti baadhi ya wanachama wa vikundi vya VICOBA kutoka mitaa ya Joshoni na kambarage wamesema kwa sasa wanakosa imani na benki hiyo ya VICOBA kutokana na viongozi wao waliohusika kutuma fedha kupitia benki ya Posta kutowapa majibu ya kuridhisha juu ya lini wanapatiwa mikopo.

Katibu wa kikundi cha kambarage Bi Magreti Mng'ong'o amekiambia kituo hiki kuwa kikundi chake kilihamasishwa kujiunga na VICOBA kupitia mratibu wa VICOBA kata Ester Mfikwa kabla ya kutuma fedha katika benki ya VICOBA makao makuu kupitia benki ya Posta kwenye akaunti na zaidi ya wiki 7 zimepita tangu fedha hiyo itumwe licha ya utaratibu kuonesha kuwa fedha hiyo ingetakiwa kuwafikia walengwa baada wiki moja.

Akizungumza na kituo hiki kwa njia ya simu kutokea jijini Dar es salaam Rais wa VICOBA nchini Bi. Devotha Likokola amesema kuwa tatizo hilo limekuwa likisababishwa na vikundi hivyo kushindwa kutimiza masharti ya kupata mikopo.

Likokola pia amewasukumia lawama waratibu VICOBA mikoa nchini kutotoa elimu kwa wanachama juu ya namna ya kupata mikopo pamoja na masharti ya kupata mikopo uelewa wa vikundi umeonekana kuwa mdogo.

Bi Likokola pamoja na kukiri mapungufu ya benki yake amekana kukitambua kikundi cha VICOBA Kambarage kwa madai kuwa hajawahi kupokea fedha wala maombi ya mkopo kutoka katika kikundi hicho jambo ambalo linawaweka njiapanda wanachama na viongozi waliotuma fedha na kushindwa kujua cha kufanya kwa kuwa wametuma zaidi ya shilingi milioni moja ili wapatiwe mkopo.