
Mtendaji Mkuu wa Kundi la Makampuni ya Calderbeg, ambayo makao makuu yake yapo nchini Uingereza, Bw. Apollo Temu, amesema kwa sasa kampuni hiyo inatoa mafunzo kwa wataalamu wa Kitanzania juu ya namna ya kuandaa, kusimamia na kuendesha miradi mikubwa ya nishati ya gesi, hasa baada ya nchi kuanza kuvuna maliasili hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Kwa mujibu wa Temu, kampuni yake imewaleta nchini wataalamu waliobobea kwenye fani za mafuta na gesi, ambao wanawafundisha wale wa Tanzania katika masuala ya kodi, mahesabu, utaalamu wa kompyuta na hata namna ya kusimamia miradi mikubwa ya gesi, ili kuhakikisha mapato yatokanayo na sekta hiyo yanainufaisha nchi na sio wawekezaji wa kigeni kama ilivyo hivi sasa.
Aidha, Temu amesema mafunzo hayo yanalenga kuunga mkono wazo la Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kutaka wazawa wajengewe uwezo ili wawe na ujuzi na kuunganisha mitaji yao, hatua itakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika kuendeleza uchumi na rasilimali za mafuta na gesi.