Jumamosi , 7th Aug , 2021

Rais aliyemaliza muda wake kwenye awamu iliyopita ya kuliongoza Shirikisho la soka nchini 'TFF', Wallace Karia ametangazwa kuwa mshindi wa Uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo kwa awamu nyingine ya miaka minne ya Uongozi kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.

Rais wa Shirikisho la soka nchini, Wallace Karia.

Rais Karia ameshinda uchaguzi huo leo Agosti 7, 2021 jijini Tanga kwa kupata kura 81 za kuidhinidhwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF ikiwa ni asimilia 100 ya ushindi na kuweka rekodi ya kuwa Uchaguzi wa kwanza kwenye historia ya soka nchini tokea uongozi wa soka kuwa shirikisho kupata rais aliyepita kugombea pekeeake na kupata ushindi.

Na kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa TFF, Kiomboi Kibanda alisema kabla ya uchaguzi huo kuanza kuwa, kwa mujibu wa kanuni ya 19 (18) ya Uchaguzi Mkuu, endapo Kuna mgombea mmoja kwenye nafasi yoyote ya kuchaguliwa, Mkutano Mkuu utamuidhinisha. 

Baada ya kueleza hayo, wajumbe wote walijibu ndiyo kwa pamoja kujibia kuwa wapo tayari kumpitisha mgombea huyo kuwa rais wa TFF na hakuna aliyejibu hapana hata mmoja.

Karia aliliongoza Shirikisho hilo kwa awamu iliyopita ya miaka minne kuanzia mwaka 2017 hadi 2021 hivyo ataliongoza tena Shirikisho kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.

Na katika Matukio mengine yaliyojiri kwenye mkutano mkuu huo unaofanyika Jijini Tanga, ni kwamba, Abdallah Bulembo ametolewa kuwa Mjumbe wa baraza la wadhamini wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF kufuatia kupeleka masuala ya uchaguzi  mahakamani.