Jumatano , 4th Aug , 2021

Louis van Gaal ametangazwa kuwa Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Uholanzi kwa mkataba wa mwaka mmoja akichukua nafasi ya Frank de Boer aliyeachana na timu hiyo baada ya michuano ya Euro 2020, na sasa Van Gaal atakiongoza kikosi hicho kwenye michezo ya kufuzu kombe la Dunia mwaka 2022.

Louis Van Gaal

Hii inakuwa ni mara ya tatu Van Gaal anachukua jukumu la kukiongoza kikosi cha Uholanzi awali alikiongoza kikosi hicho kati ya mwaka 2000 hadi 2001 na kisha mwaka 2012 hadi 2014 na sasa emerejea tena.

'’Soka la Uholanzi limekuwa moyoni mwangu na kufundisha timu ya taifa, kwa maoni yangu ni nafasi muhimu ya kusogeza mbele soka letu. Kwa kuongezea, ninaona ni heshima kufundisha timu ya taifa ya Uholanzi." Alisema Van Gaal katika taarifa iliyotolewa na shirikisho la soka la Uholanzi.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 69 ataanza kibarua rasmi mwezi Septemba ambapo atakuwa na michezo mitatau ya kufuzu fainali za kombe la Dunia itakayofanyika Qatar 2022, na anarejea tena kwenye mikikimiki ya soka kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2016 baada ya kufutwa kazi na Manchester United.

Na katika vipindi viwili vilivyopita Van Gaal alikiongoza kikosi cha the Oranje kwenye michezo 43, ambapo alikiongoza kupata ushindi kwenye michezo 27 sare michezo 11 na alifungwa michezo 5, na mafanikio makubwa ilikuwa kukifikisha kikosi hicho hatua ya nusu fainali kwenye michuano ya kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil.