
Alexander Zverev akionesha medali aliyopata baada ya kumfunga Karen Khachanov wa Urusi kwa seti 2-0 jioni ya jana Agosti 1, 2021 na kushinda fainali hiyo kwa upande wa tenisi ya wanaume.
6 – Ni idadi ya timu zilizofuzu moja kwa moja kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Olympic nchini Japan kwa upande wa mpira wa kikapu huku timu mbili, Ujerumani na Argentina zikifuzu wakiwa best loosers kufuatia Argentina kuwafunga wenyeji Japan kwa Alama 97-77 na Slovenia walipowafunga Hispania 95-87 kwenye michezo jioni ya jana.
Michezo mine ya hatua ya robo fainali yote inataraji kuchezwa Agosti 3 mwaka huu ambapo, Italy itacheza na Ufaransa, Slovenia watawavaa Wajerumani, Hispania watacheza na mabingwa watetezi, timu ya taifa ya Mareakani ilhali Australia wataungurumishana na Aregentina.
5 - Ni idadi sawa ya mashuti yaliyolenga lango kwa Arsenal na Chelsea kwenye mchezo wao wa kirafiki uliochezwa usiku wa jana kwenye dimba la Fly Emirates ambapo Chelsea ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.Mabao ya Chelsea yalifungwa na Kai Haverts dk26 kabla Granit Xhaka kusawazisha dk69’ na Tammy Abraham Kufunga bao la ushindi dk72.
Alipokuwa anazungumza na wanahabari mara baada ya mchezo huo kumalizika, kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amefunguka kwa kusema kiungo wake Granit Xhaka atasalia Gunners licha ya kuwa na tetesi za nyota huyo kutaka kutimkia klabu ya AS Roma ya nchini Italia huku akigusia hali ya Thomas Partey kuwa si nzuri kwa sasa baada ya kupata majeraha mchezoni.
4 - Ni jumla ya penalti za ushindi walizopiga timu ya Kaizer Chiefs dhidi ya Orlando Pirates waliofunga penalti 3 na Kaize Chiefs kuibuka kuwa mabingwa wa kikombe cha Carling Black Label wa mwaka 2021 nchini Afrika Kusini kwa ushidni wa penalti 4-3 baada ya sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 za mchezo.
Pirates walikuwa wa kwanza kupiga penalty, Deon Hotto, Kabelo Dlamini na Richard Ofori wakifunga huku Ntsikelelo Nyauza na Wayde Jooste wakikosa ilahli kwa upande wa Kaizer Chiefs, Daniel Cardoso, Bernard Parker, Phathutshedzo Nange wakifunga, Sabelo Radebe pekee ndiye aliyekosa na Kgaogelo Sekgota akafunga penalty ya mwisho na kuwa shujaa wa mchezo.
3 - Ni idadi ya wachezaji wanaohusishwa kusajiliwa na klabu ya wekundu wa msimbazi Simba kwa mujibu wa vyanzo vya kikachero. Wachezaji hao ni mlinzi wa kulia wa KMC, Israel Patrick Mwenda ambaye ni nahodha wa mmabingwa wa CECAFA 2021 timu ya taifa ya Tanzania U23.
Wachezaji wengine ni mlinzi wa kushoto wa zamani wa klabu ya Mtibwa Sukari ambaye sasa anatoka klabu ya Youssoufia kutoka nchini Morocco, Nickson Kibabage na mlinzi wa kati wa Abdulmajid Mangalo aliyekuwa nahodha wa kabu ya Biashara United Mara msimu uliopita na kuiongoza kushika nafasi ya nne na kuweka rekodi ya kushiriki michuano ya Shirikisho barani Afrika.
2 – Ni Idadi ya magoli yaliyofungwa kwenye siku ya ufunguzi wa michuano ya CECAFA KAGAME CUP kwenye mchezo ambao Yanga walitoka sare ya bao 1 dhidi ya timu ya Nyasa Big Bullet kutoka nchini Malawi.
Bao la ufunguzi wa michuano hiyo liliwekwa kimiani na mshambualiaji wa Yanga Waziri Shemtembo aliyefunga bao hilo dk 8 kabla ya Chiukepo Msowoya wa Nyasa kusawazisha dk30’ kwa mkwaju wa penalty kufuatia madhambi yalioyochezwa na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na dk89’ kushuhudia mlinda mlango wa Yanga, Ramadhani Kabwili akioneshwa kadi nyekundu.
Tukisalia na Wanajangwani, Jana wamethibitisha kumsajili mshambuliaji Fiston Kayala Mayele kutoka AS Vita ya DR Congo pamoja na winga Dickson Ambundo kutoka Dodoma Jiji ambaye alianza kwenye kikosi cha kwanza cha mchezo huo.
Michuano hiyo inatazamiwa kuendelea tena siku ya leo Agosti 2, 2021 ambapo Le Messager FC itacheza na KMKM ya visiwani Zanzibar saa 10:00 jioni wakati KCCA FC ya nchini Uganda itavaana na Azam FC saa 1:00 usiku kwenye dimba la Chamazi.
1 – Ni idadi ya medali ya dhahabu iliyoenda nchini Ujerumani kwa upande wa tenisi kwenye michuano ya Olympic inayoendelea nchini Japan, na hii ni mara baada ya mcheza tenisi anayeshikilia nafasi ya 5 duniani kwa upande wa wanaume, Alexander Zverev mwenye miaka 24 kupata ushindi kwa kumfunga Karen Khachanov wa Urusi anayeshika nafasi ya 25 duniani.
Zverev ameshinda jumla ya seti mbili kwa sifuri dhidi ya Khachanov mwenye miaka 25 baada ya kuongoza 6-3 na 6-1 kwenye mizunguko miwili. Baada ya kushinda medali hiyo, Zverev ameeleza hisia zake za furaha kwa kusema anajisikia fahari kuwa mjerumani wa kwanza kutwaa medali hiyo kwa upande wa tenisi ya wanaume na medali ya dhahabu ya kwanza kwake.