
Wakati watanzania wakiadhimisha miaka 53 ya uhuru wa Tanganyika watumishi wa umma mkoani Tabora wametakiwa kuadhimisha miaka hiyo kwa kutoa huduma stahiki kwa wananchi ili kuwawezesha ili kukabiliana na changamoto za kimaisha, zikiwemo huduma bora za afya, elimu maji na ardhi.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Tabora Bw. Suleimani Kumchaya wakati akiwahutubia wakazi wa manispaa ya Tabora katika viwanja vya sanamu ya baba wa taifa hayati Julius Nyerere, ambapo amesema kuwa, wananchi wanaweza kukinai uhuru wao kutokana na huduma wanazozipata.
Aidha katika hatua nyingine Bw. Kumchaya amesema kuwa, kuelekea uchaguzi mkuu wa serikali za mitaa, wananchi wanatakiwa kufanya kampeni za staha, ambazo zinavutia kuliko kujiingiza katika chuki na fitina ambazo hazijengi bali zinaleta mfarakano.
Awali msimamizi mkuu wa manispaa ya Tabora mkurugenzi Bibi Spora Liana amesema kuwa, mpaka sasa hakuna changamoto ambazo zimejitokeza, huku akiwataka wananchi wa manispaa hiyo kudumisha mshikamano ambao upo hadi siku ya uchaguzi hapo tarehe 14 Desemba 2014.