Jumatatu , 24th Mei , 2021

Msaada wa vifaa vya michezo vilivyotolewa na kampuni ya kubashiri matokeo ya Meridian Bet umeipa mzuka timu ya Lenster senior League (LCL) wa kushinda ubingwa tena wa Ligi Kuu ya watu wenye ulemavu itakayoanza Juni mwaka huu.

Timu ya watu wenye ulemavu ya LCL ikikabidhiwa vifaa vya michezo na Meridian Bet

Timu hiyo yenye wachezaji saba wa timu ya taifa imekabidhiwa msaada wa jezi, vikinga ugoko, njumu, mipira na soksi vilivyotolewa na Meridian Bet.

Meneja wa Meridian Bet, Ernest John  na Meneja Mwendashaji Mkuu  Tanzania, Corrie Borman walikabidhi msaada huo katika hafla fupi iliyofanyika makao makuu ya Meridian Bet na kueleza kuwa ni muendelezo wa kampuni yao kusaidia jamii yenye uhitaji nchini.

Nahodha wa LCL, Alphan Athuman aliyeambatana na wachezaji wengine na uongozi wa timu amesema msaada huo ni chachu kwao kufanya vizuri na kuuahidi uongozi wa Meridian Bet kurejea na kombe mwishoni mwa msimu baadae mwaka huu.