
Kocha wa Manchester City Pep akishangilia na wachezaji wake
Mabao mawili ya Riyad Mahrez ya dakika ya 11 na 63 yalitosha kuipa ushindi wa nabao 2-0 Manchester City dhidi ya PSG kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali ya michuano hiyo, na kuifanya City kufuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1.
Baada ya mchezo huo kumalizika Pep Guardiola ambaye huu ni msimu wake wa tano akiwa na kikosi hicho amesema,
“Haya ni maajabu. Watu wanaamini ni rahisi kufika kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa. Kufikia fainali sasa kuna maana ya kile tumefanya katika miaka minne au mitano iliyopita, nina mshukuru mmiliki wa timu, mwenyekiti na wafanyikazi wote wa klabu. Klabu hii inahusu watu wote wanaofanya kazi nyuma ya pazia, sio pesa tu.” alisema Guardiola
Kwenye misimu minne iliyopita Manchester City chini ya Guardiola imetolewa mara tatu kwenye hatua ya robo fainali ambapo walitolewa na vilabu vya Liverpool, Tottenham na Olympique Lyon na katika msimu wake wa kwanza baada ya kujiunga na matahiri hao wa jiji la Manchester msimu wa 2016-17 walitolewa hatua ya 16 bora na AS Monaco ya Ufaransa
Kocha huyo raia wa Hispania nae atacheza fainali yake ya kwanza ya ligi ya mabingwa baada ya kipindi cha miaka 11, mara ya mwisho Pep kuiongoza timu katika mchezo wa fainali ya michuano hiyo ilikuwa mwaka 2011 akiwa na kikosi cha FC Barcelona na alishinda fainali hiyo kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Manchester United.