Mkurugenzi wa halmashauri ya Chato Bw. Clement Berege.
Akizungumza na Ea Radio, katibu wa chama cha mapinduzi (CCM) wilayani humo, Khamis Mkaruka, amesema lawama za kudorora kwa zoezi hilo zinamwangukia mkurugenzi huyo kwa kushindwa kutoa matangazo mbalimbali ya kuwahamasisha wananchi wenye sifa kujitokeza kwa wingi ili kujiandikisha.
Mkaruka amesema kama kiongozi wa chama, ametimiza wajibu kwa kuwahamasisha wanachama na mashabiki wa chama chake kwenda kujiandikisha, lakini wanakwamishwa na mkurugenzi Berege.
Kwa upande wake, katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Chato, Mange Ludomya, amesema inawashangaza kuona mkurugenzi anawapuuza wananchi kujiandikisha katika daftari la kupigia kura, hatua inayoweza kusababisha wengi kukosa haki yao ya msingi ya kuwachagua viongozi wanaowataka.
Hata hivyo, mkurugenzi huyo alipotafutwa na Ea Radio, hakuweza kupatikana ili kutolea ufafanuzi lawama hizo za vyama vya siasa.