Pichani ni Rais Dkt John Magufuli akiwa amebeba Ngao na Mkuki, kuashiria kukabidhiwa hatamu za uongozi.
Magufuli baada ya kuapishwa alitoa hotuba fupi ambayo sehemu yake ilieleza adhma ya serikali yake pamoja na mambo mengine kuwa ni kuwaletea wananchi maendeleo, usimamizi bora wa rasilimali pamoja na kuimarisha uchumi.
Miongoni mwa rekodi ambazo Magufuli amezivunja ni pamoja na kuapishwa leo tarehe 5 Novemba 2020 sawia na tarehe ambayo alipishwa katika muhula wa kwanza mwaka 2015.
Rekodi nyingine ni kuwa Rais wa kwanza barani Afrika kutosafiri nje ya bara hilo tangu tarehe ya kuapishwa katika muhula wa kwanza hadi tarehe ya kuapishwa katika muhula wa pili.
Pia Magufuli anakuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuapishwa nje ya Jiji la Dar es Salaam na wa kwanza katika Jiji la Dodoma yaani Makao Makuu ya nchi na serikali. Pia kuwa Rais wa kwanza kula kiapo cha Urais, Taifa likiwa katika uchumi wa kati.
Rekodi nyingine ni pamoja na kuwa Rais wa kwanza nchini kushinda kinyang'anyiro cha Urais kwa asilimia ndogo zaidi katika muhula wake wa kwanza na kupata kura nyingi zaidi katika mbio za kusaka muhula wake wa pili (Magufuli 2015 kura 8,882,935 sawa na 58.46% na 2020 kura 12,516,252 sawa na 84%) tofauti na watangulizi wake.
Lakini Magufuli historia inamfananisha na Marais wenzake waliomtangulia mathalani katika eneo la kushinda mihula miwili katika nafasi ya Urais tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini 1992 ambapo Marais waliomtangulia ni pamoja na Benjamini Mkapa (1995-2005), Jakaya Kikwete (2005-2015).