Mshambuliaji kinda wa Simba, Rashid Juma akionesha makeke yake dimbani.
Nyota huyo aliyepewa nafasi kubwa ya kucheza wakati Simba ilipokuwa ikinolewa na kocha Patrick Aussems, ambaye aliondolewa mwanzoni mwa msimu uliopita, amekuwa kwenye wakati mgumu chini ya Sven Vandenbroeck ambaye hajawa na matumizi naye katika kikosi chake.
''Nilikuwa sipati nafasi ndani ya Simba kutokana na matakwa ya mwalimu, kocha anachotaka ndicho kilichosababisha nikose nafasi, ikizingatiwa timu inawachezaji wengi wazuri ambao wamenizidi mimi, kwa uhitaji wa mwalimu mimi nisingeweza kucheza'', amesema.
Aidha Rashid Juma ameeongeza kuwa, ''Mimi ndiye niliyeamua kuondoka, nilimfuata mwalimu na kumwambia kuwa naomba niende kwenye klabu nyingine ili nikapate muda zaidi wa kucheza na Sven aliridhia''.
Alipoulizwa juu ya ushauri gani anatoa kwa wachezaji ambao wapo katika vilabu vya Simba, Yanga na hata Azam FC ambazo haziwapi nafasi ya kucheza na wao hawataki kuondoka, Rashid Juma alisema kila mmoja ana uamuzi wake.
''Siwezi kutoa ushauri kwa mchezaji yoyote ambaye bado yupo Simba, Yanga na hata Azam FC na hapati nafasi, kwasababu huwezi jua anakaa huko na hatujui anachopata hivyo kila mmoja ana chaguo lake''
Rashid Juma amekua na mchango mkubwa katika klabu ya Polisi Tanzania ambapo alifunga bao zuri na la ushindi dhidi ya Namungo huko mkoani Lindi na hadi sasa maafande hao wapo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania bara.