Alhamisi , 3rd Oct , 2019

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na watoto Ummy Mwalimu, amewataka watanzania kuzipuuzia taarifa za uongo, zinazoenezwa katika mitandao ya kijamii kwa madai ya kwamba Tanzania imekuwa ikificha taarifa za uwepo wa ugonjwa wa Ebola hapa nchini.

Waziri Ummy

Waziri Ummy ametoa taarifa hiyo leo Oktoba 3, 2019, Jijini Dar es Salaam, wakati akitoa taarifa ya hali ya afya nchini Tanzania pamoja na mwenendo wa magonjwa 14 ya mlipuko yanayofuatiliwa kwa ukaribu zaidi ikiwemo ugonjwa wa Ebola.

''Ikumbukwe kuwa ugonjwa wa Ebola unaweza kusambaa kwa haraka na madhara yake ni makubwa na yanajulikaa Duniani kote ni ugonjwa ambao hauwezi kufichwa na Serikali inatambua madhara makubwa  ya kuficha ugonjwa hatari kama Ebola kwa wananchi'' amesema Waziri Ummy.

Aidha waziri Ummy ameongeza kuwa kwa mwezi  Septemba ni  magonjwa mawili tu ya milipuko yaliyoripotiwa ambayo ni ugonjwa wa homa ya Dengue na Surua na sio Ebola kama ambavyo imekuwa ikisemwa.

''Inaonekana kuna njama ovu za kueneza taarifa hasi dhidi ya nchi yetu, endapo atatokea mgonjwa wa Ebola tutatoa taarifa Shirika la Afya Duniani WHO'' amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy ameyataka mataifa yote kuwa,nchi ya Tanzania iko salama na haina ugonjwa huo na kwamba itaendelea kushirikiana na mashirika ya Afya Duniani katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huo.