Jumanne , 9th Sep , 2014

Ofisi ya taifa ya takwimu nchini Tanzania, leo imetoa taarifa ya kiwango cha mfumuko wa bei kwa mwezi August taarifa inayoonyesha kuwa kiwango cha mfumuko wa bei kimeongezeka kwa wastani wa asilimia 0.1.

Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Kijamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu NBS.

Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Kijamii wa NBS Bw. Ephraim Kwesigabo ametoa taarifa hiyo leo jijini Dar es Salaam na kwamba ongezeko hilo linaendana na hali ya mfumuko wa bei katika nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Bw. Kwesigabo ameongeza kuwa thamani ya shilingi ya Tanzania katika manunuzi nayo imezidi kuporomoka ambapo kila shilingi mia moja inaweza kufanya manunuzi yenye thamani ya shilingi sitini na sita nukta tisa pekee.

Wakati huo huo, Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini Tanzania (JWT) pamoja na Wizara ya Fedha na Uchumi nchini, wamekubaliana kufanya mapitio ya kodi ya ongezeko la thamani yaani VAT, kwa lengo la kupunguza idadi ya wafanyabiashara wanaostahili kulipa kodi hiyo kwa kigezo cha kipato.

Akitoa majumuisho ya mkutano wa pamoja baina ya wafanyabiashara hao na serikali pamoja na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) uliofanyika mjini Dodoma Septemba 5 na 6 mwaka huu, Mwenyekiti wa (JWT) Bw. Johnson Minja amesema katika kikao hicho pia wamekubaliana maduka ambayo hayatakuwa na mashine za EFD yataruhusiwa kuendesha biashara zao pasipo kusumbuliwa na mamlaka ya mapato.

Kwa mujibu wa Minja, jumuiya hiyo na serikali wamekubaliana kimsingi kuongeza kigezo cha mfanyabiashara anayestahili kutozwa kodi hiyo hadi mtu mwenye pato linalofikia fedha za Tanzania shilingi milioni 100 kwa mwaka, kutoka kiwango cha sasa cha shilingi milioni 40.