Jumanne , 16th Jul , 2019

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli, leo Julai 16 amefanya ziara ya kushtukiza katika gereza la Butimba Jijini Mwanza, ambapo amesikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wafungwa pamoja na askari magereza.

Rais Magufuli

Akizungumza gerezani hapo, Rais Magufuli amewatia moyo wafungwa na mahabusu katika gereza hilo na kuwaomba wavumilie kwani anazitambua changamoto zinazowakabili na kwamba atazifanyia kazi.

''Nimegundua vitu vingi hapa, kuna vitendo vingi mnafanyiwa, vingine ni vya kuombwa rushwa hayo yote nayajua, mimi naomba mnivumilie, hata sisi tuliopo hapa ni wafungwa wa baadae, kufungwa hakukunyimi wewe kupata utu wako  kibinadamu'', amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli ameeleza kuwa, anajua kama kuna watu wamefungwa kwa kubambikiwa kesi, wengine kwa kutokuongea vizuri na polisi, na kwamba yeye kama kiongozi ameyaona yote hayo na kuomba wamuache akazifanyie kazi changamoto hizo.

Aidha amemtaka Kamanda wa Polisi mkoani humo kufanya mabadiliko kwa maafisa upelelezi, ili waweze kuzifanyia kazi kesi zote za wafungwa, waliocheleweshewa na kubambikiwa kesi ili wapate haki zao.