
Waziri Kangi Lugola
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya ukaguzi, Waziri Lugola amesema wamekagua na kuona ufanisi wa namna Jeshi la polisi linavyotoa huduma kwa wananchi na kuwasikiliza maoni ya wananchi juu ya huduma wanazozipokea kutoka kwa jeshi hilo.
Amesema kituo hicho kilikuwa kinaongoza kwa kukaa na mahabusu kwa muda mrefu na leo Juni 23, 2019 amekuta mahabusu 32, ambapo mahabusu 11 wanaohusika na kesi za mauaji na baadhi yao wamekaa magereza kwa miaka 7 na baadaye kurudishwa kituoni hapo ili kuweza kufutiwa kesi zao ila hadi sasa wapo kituoni hapo kwa miezi 6 jambo ambalo sio sahihi na amezungumza na viongozi wa vituo hivyo na tatizo hilo litatatuliwa.
Kuhusiana na suala la mawasiliano hasa katika suala hilo la mahabusu kukaa vituoni muda mrefu, amelichukua kama changamoto na kuhusiana na changamoto ya dhamana amempa maelekezo Mkuu wa Kituo cha Polisi kulishughulikia na kupiga marufuku kauli ya 'utakaa ndani hadi Jumatatu' ili hali kuna wadhamini.
Amesema kutokana na malalamiko ya vijana wengi wa bodaboda, ameagiza vyombo husika kuwa bodaboda zinazostahili kukamatwa ni zile zilizohusika na uharifu, zilizohusika na ajali, zilizopotea na kuonekana na zile zilizookotwa, zingine zinazokamatwa na makosa kama kupakia abiria zaidi ya mmoja maarufu kama 'mshikaki' na kutovaa kofia ngumu, mshtakiwa anaweza kutozwa faini ambayo italipwa ndani ya siku saba.