Ijumaa , 22nd Aug , 2014

Madaktari wa magonjwa ya binadamu, wameishauri wizara ya afya na ustawi wa jamii kuhakikisha inapanua wigo wa uboreshaji wa huduma za maabara ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii nchini Tanzania Dkt Seif Rashid.

Akizungumza katika majadiliano ya madaktari wa mkoa wa Arusha mtaalamu wa magonjwa ya kina mama Dkt. Frank Msuya amesema wananchi wengi hususani wa kipato cha chini wamekuwa wakikosa tiba sahihi kutokana na kukosa vipimo vya uhakika vinavyoonesha ugonjwa.

Kwa upande wake mtaalamu wa maabara kutoka maabara ya Lancet iliyozinduliwa hivi karibuni jijini Arusha Bw. Ahmed Calleb amesema siku zote utendaji kazi bora wa daktari unafanikishwa na majibu sahihi ya vipimo vya mgonjwa.

Wakati huo huo, Kamishna wa Jeshi la Magereza nchini Tanzania John Minja amesema kumekuwepo na ongezeko kubwa la mahabusu katika magereza ambao wengi wao wanatuhumiwa kutenda makosa ya jinai.

Akiongea katika kongamano la siku mbili lililoandaliwa na Sekretarieti ya Msaada wa sheria (LAS) kamishna wa huduma za kisheria wa jeshi la magereza, Deonice Chamulesile kwa niaba ya kamishna wa jeshi hilo nchini amesema idadi ya mahabusu nchini imeongezeka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na idadi ya magereza yaliyopo.

Chamulesile amesema kufuatia hali hiyo ametoa wito kwa taasisi zinazotoa msaada wa kisheria nchini kujikita zaidi katika kutoa huduma hiyo katika maeneo mbalimbali nchini hususani kwa watuhumiwa waliopo katika vizuizi ili kupunguza idadi ya mahabusu.