
Wanawake wenye makalio makubwa nchini Uganda.
Wamesema kuwa lengo lao sio kutumia shindano la 'Miss Curvy Uganda' kuvutia watalii kuja nchini humo, bali wanataka kuwapa motisha wanawake wenye maumbo makubwa ili nao pia wajiamini kuwa ni warembo.
Siku mbili zilizopita spika wa bunge nchini humo, Rebecca Kadaga aliyapinga vikali mashindano hayo lakini amebadili msimamo wake baada ya kupokea ufafanuzi huo na ameahidi kuunga mkono juhudi zao na kutoa ufafanuzi kwa bunge ili kuondoa fikra kwamba mashindano hayo ni ya aibu kwa mwanamke.
Waziri wa utalii nchini Uganda, Godfrey Kiwanda alipendekeza kuwepo kwa onesho la wanawake wenye maumbo makubwa ili kuvutia wageni zaidi wanaoitembelea nchi hiyo.
Akizungumza katika uzinduzi wa shindano hilo, waziri huyo wa Utalii alisema kuwa,"litakuwa tukio la kipekee ambalo litawaonesha mabanati wakionesha maumbo yao mazuri yaliyo nona".
Kauli hiyo ilizua mjadala mkali hasa katika mitandao ya kijamii huku baadhi ya watu wakimshutumu waziri Kiwanda kwa kuzungumza vibaya juu ya wanawake wanene kuwa wana nyama huku mwanamke mmoja akihoji kama ingewezekana basi wawekwe bustanini ili watazamwe kama wanayama watendewavyo.