
Kocha, Jose Mourinho
Kwa mujibu wa tetesi mbalimbali, kocha huyo wa kireno huenda akaelekea kwa vigogo wa nchi ya Ureno, Benfica, kufuatia kumtimua kocha wake, Rui Victoria hivi karibuni.
Rui Victoria alitimuliwa baada ya kufungwa mabao 2-0 katika mchezo wa ligi kuu ya Ureno 'Primeira Liga' dhidi ya Portimonense, ambapo hivi sasa vigogo hao wako nafasi ya nne wakiwa nyuma kwa pointi 7 mbele ya kinara FC Porto.
Kwa mujibu wa ripoti ya mtandao wa AS, umeripoti juu ya uwezekano wa Jose Mourinho kuwa kocha mpya ajaye wa Benfica.
Lakini mpaka sasa, Mourinho hajaonesha nia yoyote ya kutaka kurejea kufundisha Ureno baada ya kufanya vizuri na klabu ya FC Porto mwaka 2003.
Katika kipindi ambacho aliifundisha Porto, alishinda taji la Klabu Bingwa Ulaya, mataji mawili ya ligi ya Ureno, kombe la UEFA, makombe mwili ya Ureno pamoja na Portuguese Super Cup mara mbili. Pia alifanikiwa kushinda tuzo ya kocha bora wa Dunia kwa miaka miwili, 2003 na 2004.
Mourinho aliwahi kuifundisha Benfica mwanzoni mwa mwaka 2000 lakini aliondoka baada ya michezo 9 tu ya ligi. Alikabidhiwa mikoba ya kuwa kocha mkuu baada ya kocha Jupp Heynckes kuondoka mwanzoni mwa msimu, japo na yeye hakudumu kwa muda mrefu kutokana na kutokuwa na maelewano juu ya mkataba na uongozi wa klabu.